Naanza kwa kumpongeza sana mheshimiwa Mohammed Dewji kwa uamuzi wake wa kuwekeza katika maendeleo ya soka nchini Tanzania.Huu ni uamuzi wa busara na ukarimu kwa vijana wetu ambao wananufaika kwa ajira ndani ya African Lyon.
Kwa ujumla mimi binafsi sifurahii sana mwenendo wa timu yetu katika mikimiki ya ligi kuu ya Vodacom katika misimu iliyopita.
Mwenendo unawaathiri kisaikolojia wachezaji na washabiki kwa ujumla na kujenga matumaini hasi kudumu katika chati ya timu za ligi kuu kwa sasa na wakati ujao.
Naomba menejimenti ikubali kuwa kocha mzuri bila mbinu za medani siyo uhakikisho wa kufanya vema katika mchakato wa ligi kuu ya Vodacom na mashindano mengine muhimu kitaifa na kimataifa.
Wakati hayo yakiendelea ni lazima menejimenti ya African Lyon na wadau wote tukumbuke kuwa anga la Jiji la Dar es salaam limehanikizwa na ushabiki wa Simba na Yanga na ni vigumu sana kwa timu nyingine kupenyeza kwa ufanisi ndani ya nyoyo za wakazi wa jiji la Dar es salaam.
Kwa maelezo hayo hapo juu naomba menejimenti na wadau wote wa African Lyon tukubaliane kuwa kuanzia msimu ujao wa ligi kuu ya Vodacom uwanja wa nyumbani wa timu yetu ni Namfua mkoani Singida.
Hii itakuwa fursa njema ya kuijenga timu yetu kisaikolojia kupitia washabiki wa mkoa wa Singida ambao kwa upande mmoja ni wadau wakubwa wa mheshimiwa Mohammed Dewji .
Kwa ufupi huu ndiyo mchango wangu kwa leo,lakini nipo tayari kukutana rasmi na menejimenti ya timu yetu kwa mashauriano ya pamoja.
Ray Ephraim Ndewingiya Njau Mdau wa michezo na utamaduni Dar es salaam.